mtwara regional referral hospital
(ligula RRH)

Afya ya Uzazi na Magonjwa ya Wanawake

Posted on: April 23rd, 2024


Huduma zinazotolea ni:-

KLINIKI YA NJE

Kliniki ya kuona wagonjwa wa nje hufanyika mara mbili kwa wiki, kila Jumanne na Alhamis kuanzia saa 2 na nusu asubuhi mpaka saa tisa na nusu mchana.

Kliniki hii inahudumia wagonjwa wote wanaotoka nyumbani au waliopewa rufaa kutoka vituo vya afya vya chini lakini hawahitajiki kulazwa.

Baadhi ya wagonjwa wanaotibiwa kliniki ni wajawazito wenye mimba zisizo na matatizo ya kuhitaji kulazwa, wenye matatizo ya uzazi kushindwa kushika mimba, mimba zinazotoka mara kwa mara, uvimbe katika mji wa mimba (Mfuko wa uzazi), kizazi kutokea njia ya uke, uambukizi katika njia ya uzazi (PID), kupima saratani ya shingo ya kizazi na kuiondoa katika hatua za mwanzo n.k.

Pia kliniki inaona wagonjwa walioruhusiwa kutoka wodini kwa ajili ya kufuatilia maendeleo yao baada ya matibabu.

Kupitia kliniki, wagonjwa hupangiwa upasuaji kwa wale wenye kuhitaji huduma hiyo kama vile upasuaji wa kutoa mtoto (kwa wale wenye sababu za kufanyiwa), upasuaji wa kutoa uvimbe kwenye mfuko wa uzazi (Fibroids), upasuaji wa kutoa kizazi chote, upasuaji wa kutoa uvimbe katika mayai n.k


WAGONJWA WA NDANI – KITENGO CHA AFYA YA UZAZI

Kitengo hiki kina wodi 3 ambazo ni wodi ya wajawazito, wodi ya kujifungua na wodi ya ambao wameshajifungua. Wodi hizi zote hulaza wagonjwa wenye hali mbalimbali kama ifuatavyo:

Wodi ya wajawazito – hulaza wajawazito wote wanaoanzia wiki 28 za mimba na kuendelea, wajawazito wenye matatizo ya shinikizo la damu, kifafa cha mimba, upungufu wa damu kipindi cha ujauzito, maambukizi ya njia ya mkojo kipindi cha ujauzito, kutokwa na damu kabla ya kujifungua, ugonjwa wa malaria kipindi cha ujauzito, kuvuja maji kabla ya muda wa kujifungua, wajawazito waliofanyiwa upasuaji mimba zilizopita n.k

Wodi ya wanaojifungua – tunavyo vyumba 3 vya kujifungulia na vitanda 6 vya kujifungulia, chumba kimoja binafsi cha kujifungulia. Vyumba vyote hivi hulazwa wale walioanza uchungu wa kujifungua.

Wodi ya waliojifungua  - hulazwa wagojwa waliojifungua tayari kwa njia ya kawaida na upasuaji, wagonjwa  wenye matatizo ya vidonda baada ya kufanyiwa upasuaji, upungufu wa damu baada ya kujifungua n.k

WAGONJWA WA NDANI – KITENGO CHA MAGONJWA YA WANAWAKE

Wodi hii hulazwa wagonjwa wenye matatizo mbalimbali kama vile magonjwa ya wanawake ya kutoka damu bila mpangilio maalum, mimba zinazotoka bila ya wakati, uvimbe katika mfuko wa uzazi (fibroids), matatizo ya kutoshika mimba, uvimbe katika mayai n.k

Vilevile mimba zote ambazo hazijatimiza wiki 28 kuendelea na matatizo mengine ya ujauzito kama vile kutapika kupita kiasi, malaria katika kipindi cha ujauzito, maambukizi katika njia ya mkojo, shinikizo la damu kipindi cha ujauzito kwa mimba chini ya wiki 28 n.k


DAKTARI KUONA WAGONJWA WODINI

Katika kila wodi, wagonjwa hupitiwa na kuonwa na daktari na manesi kitanda kimoja mpaka kingine kila siku Jumatatu mpaka Jumapili.

Na kila Jumatano kundi la madaktari, manesi wakiongozwa na daktari bingwa hupita na kuwaona wagonjwa wodi zote .

 

UPASUAJI

Wagonjwa wanaoonwa na kupangiwa upasuaji, wanafanyiwa upasuaji kila siku ya Jumatatu na Ijumaa. Na wagonjwa hao hulazwa siku moja kabla ya upasuaji yaani Jumapili na Alhamis.

Lakini kwa upasuaji wa dharura, huduma ya upasuaji inafanyika wakati wowote na siku zote.


MAFUNZO

Idara yetu pia inashiriki katika kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaotoka vyuo vya afya karibu na Hospitali yetu kama vile wanafunzi wa mafunzo ya Utabibu na manesi.


ELIMU

Elimu ya kujikumbusha na kuongeza uzoefu hutolewa kila siku ya Alhamis katika idara kuanzia saa 2 kamili asubuhi mpaka saa 3 kamili asubuhi.

Hii inasaidia kufanya wafanyakazi katika Idara hii kuendelea kuwa na uwezo wao mzuri katika kazi, maarifa Zaidi, ujuzi na matokeo mazuri katika kutoa huduma kwa wagonjwa, jamii na idara kwa ujumla.