mtwara regional referral hospital
(ligula RRH)

Upasuaji (Surgical)

Posted on: July 20th, 2024

Idara ya upasuaji ni moja ya idara kuu za Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ligula,Historia ya idara hii inaenda pamoja na historia ya hospitali ambayo ilianzishwa kama kituo cha kutolea huduma kwa majeruhi wa vita vya ukombozi vilivyoongozwa na chama cha FRELIMO Msumbiji.Utoaji wa huduma ya matibabu kwa majeruhi ni moja ya kazi za idara ya upasuaji.Idara imeendelea kukua hatua kwa hatua hadi sasa imefikia vitanda 42.Idara inatoa huduma za upasuaji aina mbalimbali kama vile ngiri aina zote,ngiri maji,bawasiri,upasuaji wa tumbo,utumbo mdogo na mpana,maradhi ya mfuko wa nyongo na ini,uvimbe kwenye shingo,upasuaji wa kurekebisha viungo,upasuaji njia ya mkojo na baadhi ya maradhi ya mifupa na upasuaji wa mishipa ya fahamu.Kwa kipindi cha miaka mitatu idadi ya wagonjwa wa upasuaji ambao vidonda vyao viliingiwa na bakteria  na kupata usaha umekuwa chini ya asilimia moja na hivyo kuifanya hospitali ya Rufaa ya Ligula kuwa ni chaguo la wananchi wa Mtwara.

Idara ya upasuaji ina daktari bingwa mmoja na madaktari watatu walio na ari kubwa na wanaofanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.Idara ina fanya  upasuaji siku ya Jumanne na Alhamisi na Kliniki za idara zinafanyika  siku za Jumatatu na Jumatano.Hivi karibuni idara imeanzisha idara ya upasuaji pua koo na sikio baada ya daktari mmoja kukamilisha masomo yake ya uzamili.Idara ina mipango ya muda mfupi ya kupunguza hali ya ukosefu wa huduma za kibingwa hospitalini hapa kwa kuwaalika madaktari bingwa kutoka hospitali za Rufaa za kanda na Taifa.Wagonjwa wenye uhitaji wa madaktari bingwa wataandaliwa na kupewa rufaa kwenda hospitali kuu za kanda na Taifa au kusuburia wataalam watakaoalikwa na hospitali kuja kuwaona wagonjwa hawa hospitalini Ligula.Idara pia inafanya usimamizi shirikishi kwenda hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya vya wilaya na halmashauri za mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Timu ya Uendeshaji Huduma za Afya ya Hospitali.Timu ya Usimamizi Shughuli za Afya Mkoa na Mamlaka za serikali za Mitaa.

Mpango wa muda mrefu na wa kudumu ni kuwashawishi madaktari waweze kwenda kusoma masomo ya uzamili katika fani za upasuaji mifupa,njia ya mkojo,upasuaji wa jumla,ganzi,masikio pua na koo,macho na upasuaji wa kurekebisha viungo kwa muda mfupi uwezekanavyo.Idara inalengo la kuifanya iwe ya mfano wa kuigwa katika Mkoa wa Mtwara katika kufanya tafiti zenye tija,matumizi ya teknolojia,usalama wa mgonjwa wakati wa tiba na mafunzo.